Dereva teksi, Idd Ayoub, amekutwa ameuawa kinyama kwa kupigwa risasi katika paji lake la uso na watu wasiofahamika na kuachwa akiwa ndani ya gari lake katika eneo la Sinza D, jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia tukio hilo jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema alipata taarifa ya tukio hilo jana saa 12:40 asubuhi.
Alisema marehemu huyo mkazi wa Makuti Magomeni, alikutwa akiwa amekufa katika gari lake lenye namba za usajili T444BYK ambayo ni teksi yenye alama ya Wilaya ya Kinondoni na ubavuni ikiwa na namba 3300.
Kamanda Kenyela alisema kituom cha teksi hiyo ni eneo la Usalama na baada ya wahusika kufanya tukio hilo la kinyama, waliondoka na funguo za gari na kumwacha marehemu ndani ya gari.
Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi na kwamba waliokota ganda moja la risasi ya bastola inayosadikiwa ilitumika kumuua dereva huyo.
Hata hivyo, Kamanda Kenyela alisema chanzo cha mauaji bado hakijafahamika na kwamba jeshi la polisi linaamini yatakuwa na sababu au kisasi.
"Kama wangekuwa ni majambazi wamefanya tukio hilo, wangeondoka na gari hilo ila wameliacha na kuondoka zao hapo kutakuwa na kitu na ndiyo maana tunafanya uchunguzi kuwabaini waliohusika," alisema.
Kamanda Kenyela alisema watu ambao wanamfahamu marehemu walisaidie Jeshi la Polisi kueleza kuwa mara ya mwisho alionekana akiwa na watu gani ili kufanikisha uchunguzi wao na hatua zichukuliwe kwa haraka.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa serikali za mtaa katika eneo la Sinza D, Richard Kalokola, alisema alipatiwa taarifa juu ya tukio hilo na ndipo walipochukua hatua ya kuwaita polisi kwenda kuliangalia gari hilo.
Alisema gari hilo ambalo linaonyesha mmliki ni Hagai Makasendo, baada ya kuona limeegeshwa kwa muda mrefu, ndipo walipoitilia shaka na kutoa taarifa katika kituo cha polisi ambao walifika na kulifungua na kumkuta dereva huyo ameshakufa.
Akizungumza na NIPASHE jana, kaka wa marehemu, Yahya Maneno alisema mdogo wake ana miaka 32 na ameacha mke na watoto wanne huku wa mwisho akiwa na umri wa miezi sita.
Alisema wanatarajia kusafirisha mwili huo kwenda Tanga kwa maziko, lakini wanasubiri taratibu za Polisi.
Alisema kwa mujibu wa taarifa alizopata kutoka kwa madereva wenzake ni kwamba juzi usiku aliagana na wenzake kwenye kituo chao cha kazi, lakini yeye (Iddi), alitania kwamba anasubiri 'kichwa' cha mwisho mwisho.
Dereva ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema katika kusubiri, ndipo walitokea akina dada wawili ambao walidai wamekabwa na hawakuwa na fedha ya kutosha, hivyo waliomba kupelekwa Saba Saba kwa Sh. 8,000.
Alisema akina dada hao walijieleza kwamba wanatoka viwanja vya Leaders Kinondoni na walikabwa na watu wasiowafahamu, lakini alikataa kuwapakia.
Alisema ndipo marehemu aliwahurumia akina dada hao na kuamua kuwapeleka kwa kiasi hicho cha fedha lakini katika hali ya kushangaza, alikutwa Sinza akiwa ameuawa.
Alisema inawezekana waliomua ni majambazi ambao walitaka kupora gari kwa sababu amekutwa akiwa kwenye kiti cha abiria badala ya kile cha dereva na tairi la kulia lilikuwa limepinda.
Aidha, alikutwa akiwa na Sh. 12,000 pamoja na simu yake ya mkononi ambayo ilitumika kutoa taarifa kwa ndugu na jamaa zake juu ya kifo hicho.
Inasadikika kwamba mauaji hayo yalifanyika alfajiri ya jana kwa kuwa hadi anatolewa ndani ya gari, marehemu alikuwa akivuja damu.
No comments:
Post a Comment