Maisha ni kupanda na kushuka! Safari ya maisha ya
muigizaji wa sinema za Kibongo, Wastara iligubikwa taswira ya faraja kidogo
huku machungu pia yakichukuwa nafasi yake.
HISTORIA YAKE KIFUPI
Wastara alizaliwa Septemba 27, mwaka 1983 huko mkoani
Morogoro. Mwaka 1987 akajiunga na Shule ya Msingi Mvomelo ‘A’ na kufanikiwa
kumaliza elimu yake ya msingi mwaka 1995.
Mkali huyo kipenzi cha watu kwenye ulingo wa sanaa, mwaka
1996 alijiunga na Sekondari ya Agricalture mkoani humo ambapo hakufanikiwa
kumaliza kidato cha nne kutokana sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake.
“Kuna rafiki yangu alikuwa anakula fedha za dada yake
sasa tukawa tunatumia naye sasa msako ulipofanyika mimi nikaonekana ndiyo
chanzo cha wizi huo mkubwa wa fedha ikabidi nitimke zangu,” anasema Wastara.
ATIMKIA MLANDIZI
Kwa kuwa darasa halikuendelea, Wastara aliamua kurudi
Mlandizi mkoani Pwani kwa bibi yake aliyekuwa akiishi maeneo hayo miaka hiyo ya
1996 baadaye kurudi tena Morogoro kusomea masuala ya madini.
Lengo la kusomea fani hiyo lilikuwa ni kumsaidia bibi
yake aliyekuwa akifanya biashara ya kuuza madini mara atakapohitimu.
Mwaka 1997, mwigizaji huyo alifanikiwa kupata mume, kwa
mara ya kwanza akaolewa na jamaa mmoja aliyejulikana kwa jina la Juma Issa
ambapo mwaka 1998 alibahatika kuzaa naye mtoto mmoja kisha ndoa hiyo
ikasambaratika kutokana na kutofautiana kwa tabia.
AKUTANA NA MAJUTO
Mara baada ya kumwagana na Juma, mwaka 1999 Wastara
alianza kuvutiwa na uigizaji baada ya kuona kazi mbalimbali alizokuwa
akizifanya mwigizaji wa kitambo, Athuman Majuto ‘King Majuto’.
Aliamua kufunga safari hadi mkoani Tanga kwa ajili ya
kusaka nafasi ya kuigiza, alipofika mkoani humo, bahati nzuri alimkuta mzee
Majuto akiwa katika harakati za kuanza kurekodi filamu ya Utaishia Kunawa. Mzee
Majuto alivutiwa na muonekano wake, moja kwa moja akamuamini acheze filamu hiyo
tena kwa nafasi ya mhusika mkuu.
“Kwa kuwa nilikuwa nikipenda anavyoigiza (Majuto),
nilitamani kuigiza vizuri ili niendelee kuigiza naye na kweli nikafanikiwa
kufanya vizuri sana kwenye filamu hiyo,” anasema Wastara.
Mara baada ya filamu hiyo kutoka, wazazi wa Wastara
walimjia juu kwa kudai filamu ni mambo ya kihuni na kumtaka aache mara moja,
akaacha.
AIBUKIA ITV
Baada ya kujiibaiba mara kwa mara kuigiza bila mafanikio
makubwa, hatimaye mwaka 2006 staa huyo wa filamu aliibukia kwenye mikono ya
Kundi la Sanaa za Maigizo la Kaole.
Hapo akaanza kuuza sura katika mchezo wa Miale ambapo
ulimpa umaarufu zaidi baada ya kuonesha umahiri wake wa kuigiza.
AKUTANA NA JENIFA MGENDI
Wastara hakudumu sana kwenye kundi hilo, alikutana na
kina Jenifa Mgendi ambaye pia walifanikiwa kuigiza naye filamu
iliyowashirikisha baadhi ya wasanii wa kitambo akiwamo Dino na wengineo.
Mwaka 2007, Wastara alifanya usahili kwenye filamu ya
mdau Ande John iliyofahamika kama Pelemende, akafaulu na kuigiza kwenye filamu
hiyo kisha zikafuata filamu nyingine kama Penina kabla ya kutimkia nchini Kongo
kufanya biashara.
AKUTANA NA SAJUKI
Aliporejea kutoka Kongo, Julai, 2007, Wastara aliitwa na
mwigizaji Shija ambaye alimuomba aigize naye filamu baada ya kumuona kupitia
kazi mbalimbali alizowahi kufanya hapo nyuma.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa Wastara kukutana na Sajuki
ambaye sasa ni mumewe wa ndoa kwani Shija alikuwa akifanya kazi zake za
uigizaji kwa kupata msaada mkubwa kutoka kwa Sajuki.
Wastara alicheza filamu kadhaa akiwa na Shija pamoja na
Sajuki hadi baadaye walipokuja kugundua kuwa matatizo ya uhusiano yaliyowakuta
(Sajuki na Wastara) yanafanana kwani kila mmoja wao alitendwa na mpenzi wake
ndipo walianzisha uhusiano wa kimapenzi.
“Eeeeh! Kazi na
dawa, tuligundua kuwa matatizo yetu yanafanana. Taratibu tukaanza uhusiano ili
kufarijiana,” anasema Wastara.
FILAMU WALIZOZALISHA
Wakiwa ndani ya umoja wao, Sajuki na Wastara,
walifanikiwa kuporomosha filamu kama Mboni Yangu, Two Brothers ambazo zilifanya
vizuri sokoni.
APATA AJALI
Wakati harakati za ndoa zikiwa zimepamba moto, mwaka 2009
Wastara alipata ajali ya pikipiki iliyosababisha akatwe mguu.
Wakati huo tayari alikuwa ameshachumbiwa na Sajuki.
Juni mwaka huohuo,
wasanii hao waliopitia changamoto kadhaa za maisha,
walifunga ndoa na kuanza rasmi maisha ya mume na mke.
Baada ya hapo, kupitia kampuni yao ya Wa-Jey waliendelea
kuzalisha filamu kama Briefcase, The Killers, Seven Days na Mboni Yangu.
APATA MTOTO
Pamoja na kumuuguza mumewe anayesumbuliwa na ugonjwa wa
uvimbe tumboni hadi sasa, mapema mwaka huu Wastara alijifungua mtoto Farheen
katika Hospitali ya TMJ jijini Dar.
MAFANIKIO
Kwenye sanaa, Wastara amefanikiwa kujulikana na watu
wengi kutokana na filamu zake zenye hisia, usafiri wa kutembelea pamoja na nyumba iliyopo Tabata jijini dar!!
No comments:
Post a Comment